Sunday, July 15, 2012

CHECK: HABARI ZA MSITU WA PANDE


Pori la Akiba la hifadhi ya Taifa lililogeuzwa msitu mateso, mauaji
Joseph Zablon
WENGI wamezoea kuuita Msitu wa Pande, lakini eneo hilo ni Pori la Akiba, lililopo  kilometa 25 kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam katika Barabara Kuu kuelekea mji wa Bagamoyo.
Pori hilo la Akiba linamilikiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, lilitangazwa kuwa la akiba mwaka 1952.
Ili kufika Msitu wa Pande kutokea katikati ya mji, utalazimika kuteremkia kituo cha daladala cha Bunju ‘B’.
Kutoka hapo kuna daladala zisizo rasmi na pikipiki (bodaboda), ambazo zinasafirisha abiria kwa kutumia barabara inayoanzia eneo hilo kupitia katikati ya msitu huo hadi eneo la Mbezi, Barabara Kuu ya Morogoro.
Pori hilo lina ukubwa wa ekari 1,226 na kilometa za mraba 15.
Lilipewa hadhi ya kuwa Pori la Akiba baada ya kuzingatia vigezo mbalimbali na tafiti tofauti kubaini kuwepo kwa viumbe hai na aina za mimea adimu, zisizopatikana maeneo mengine.
Msitu wa Pande unazungukwa na vitongoji vya Mpiji Magohe, Kibesa, Msakuzi na Mbopo.
Hata hivyo, katika miaka ya karibuni pori hilo limejipatia sifa mbaya ya kutumika kama kichaka cha kutesea watu, mauaji na vituko mbalimbali.
Sifa hiyo mbaya ya pori hilo ilianza kuvuma mwaka 2006 baada ya wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, mkoani Morogoro kuuawa na polisi katika eneo hilo kwa kilichoelezwa kuwa walidhaniwa kuwa ni majambazi.
Baada ya hapo Tume iliundwa kuchunguza tukio hilo, ikabainika kuwa waliouawa hawakuwa majambazi.
Askari waliohusika na maujai hayo walifunguliwa kesi, ambayo ilivuta hisia za wengi kutokana na unyeti wake na mazingira ya tukio lenyewe.
Mbali ya vituko vya hapa na pale vinavyoshuhudiwa na kusimuliwa na majirani wa msitu huo, mwaka huu ikiwa miaka sita tangu kuuawa wafanyabiashara wa Mahenge, pori hilo limezizima tena, baada ya kiongozi wa madaktari, Dk Steven Ulimboka kutekwa, kuteswa na kisha kutelekezwa katika msitu huo.
Wakazi wa jirani
Matukio hayo makubwa ambayo yameweza kuripotiwa na mengine mengi ambayo hayajaripotiwa, yamezua hofu miongoni mwa wakazi jirani na eneo hilo.
Wakizungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti wiki hii kuhusiana na eneo hilo, wakazi hao wanasema vitendo vya mauaji na watu kukutwa wametupwa Msitu wa Pande wakiwa hawajitambui baada ya kujeruhiwa vibaya ni vya kawaida.
Mmoja wa wajumbe wa mashina yaliyopo katika eneo hilo jirani na msitu huo, Malyesi Mawazo anasema nyumbani kwake kumegeuka mapokezi ya waliojeruhiwa na kutupwa katika pori hilo.
"Mtu asipookotwa akiwa hoi kwa vipigo, basi itakutwa maiti na wote wanaookotwa eneo la upande wa huku, wanaletwa kwangu isipokuwa huyo daktari (Ulimboka)aliyeokotwa hivi karibuni." alisema.
Mjumbe huyo anabainisha kuwa siku chache kabla ya tukio hilo la Dk Ulimboka), aliokotwa mwanamke akiwa taabani kutokana na vipigo na mambo mengine aliyokuwa amefanyiwa.
Anaeleza kuwa kutokana na hali hiyo, hofu imejengeka miongoni mwa wakazi wa eneo hilo na kwamba sasa kuanzia saa 12:00 jioni hakuna mtembea kwa miguu dereva wa pikipiki anayekubali kupita katika barabara hiyo.
Mawazo alisema ni jambo la kawaida kusikia dereva wa bodaboda amenyongwa na mwili wake kutupwa eneo hilo.
Ulinzi
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, eneo hilo halina doria wala ulinzi wa uhakika wa polisi, huku nyumba za askari wa hifadhi hiyo zikiwa mbali na barabara hiyo.
Mkazi wa eneo hilo, Abdallah Naweka alisema msitu huo umekuwa balaa kwao kwani unatumiwa vibaya na watu wanaoishi nje ya vijiji vinavyozungumza hifadhi hiyo vya Mpiji Magohe, Kibesa, Msakuzi na Mbopo.
"Kuna jamaa mfanyabiashara, mwanzoni mwa mwaka huu alitekwa na kuletwa huku akapigwa, akaporwa fedha zake na kuachiwa Sh600 mfukoni. Alijikokota hadi nyumbani kwangu na kuomba msaada," anasema Naweka.
Mmoja wawamiliki wa mashamba yanayopakana na msitu huo upande wa Mbezi anasena  vituko ni jambo la kawaida katika msitu huo.
Anasimulia kuwa siku moja alifika shambani kwake na jirani na Msitu wa Pande alishuhudia gari lililoegeshwa na watu wsiojulikana, alipolisogelea aligundua kuwa lilikuwa limeng’olewa vitu vyote muhimu.
Anaongeza kuwa siku nyingine alikuta nguo za mtu zimeachwa bila mwenyewe kujulikana aliko.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mabwepande, Abdallah Kunja anakiri kushamiri kwa vitendo hivyo, akisema vinafanywa na watu wanaotoka jijini ambao wanaonekana kuufahamu vizuri msitu huo kuliko wenyeji.
"Usiku nikisikia gari linapita najiuliza sijui kesho nitasikia nini?" anasema mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa linapopita gari usiku basi ni lazima kesho yake utasikia maiti imeokotwa au mwili umetelekezwa.
Alisema hali si nzuri kwani wahalifu hao wakishafanya walilokusudia, hawarudi na njia waliyoingilia.
“Kama wameingilia Bunju 'B', wataenda na kutokea Mbezi, hakuna gari ambalo limewahi kupita na kurudi.”Anasema.

Kunja alisema muda wa mwisho wa watu kupita eneo hilo ni kuanzia saa 12.00 jioni na hivi sasa wanaishi kwa hofu kutokana na hofu ya kukutana na matukio ya namna hiyo.
Anasema hadi sasa hajui Serikali ina mpango gani na eneo hilo kwani limegeuka kichaka cha maovu.
Alisema barabara hiyo pia inatumiwa na watu wanaoingiza bidhaa za magendo kutoka katika Bandari 'bubu' ya Mbweni ambao husafirisha mizigo hiyo hadi Mbezi na kutafuta mwelekeo mwingine, wa kwenda mikoani au kurudi mjini.
Kamanda wa polisi
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela anasema hajapata taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu katika msitu huo kiasi cha kuhitaji ulinzi maalum.
Alifafanua kuwa uhalifu unaotokea eneo hilo, unaweza kuwa ni wa kawaida kama katika maeneo mengine, hata hivyo alisema jeshi la polisi litafuatilia taarifa hizo.
 “Nipe muda nifanye ufuatiliaji, ikiwamo kuwasiliana na wakuu wa vituo vilivyopo eneo hilo, ili kujua hali halisi ilivyo kwani inawezekana kuna matukio yanafanyika lakini hayafiki ofisini kwangu,” anasema Kenyela.
Kamanda huyo aibainisha kuwa tukio la hivi karibuni la kutekwa Dk. Ulimboka na hatimaye kupigwa vibaya kisha kutupwa katika msitu huo haliwezi kuwa kigezo cha msitu huo kuwa eneo linalohitaji ulinzi maalumu. HABARI HII KUTOKA GAZETI LA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment