Thursday, May 10, 2012

MA - DC 31 NJE, 70 WAPYA, WAMO WANAHABARI, WABUNGE WA ZAMANI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya zote nchini, huku akiwatupa nje 31 na kuteua wapya 70 kati ya 133 walioteuliwa, ikiwa ni wiki moja tu tangu yafanyike mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri.

Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete amewahamisha wakuu wa wilaya 48, wakati waliobaki katika vituo vyao vya awali ni 15 tu.

Kabla ya kutangazwa jana, nafasi za wakuu wa wilaya 20 zilikuwa wazi kutoka na sababu mbalimbali, zikiwamo waliokuwa wakuu wake kuteuliwa kushika nafasi nyingine za uongozi ndani na nje ya Serikali.

Miongoni mwa wakuu wa wilaya wapya, wamo waandishi wa habari watano, wabunge wa viti maalumu na waliokuwa wabunge katika kipindi cha 2005 – 2010 ambao walipoteza nafasi zao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, 2010.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alitangaza mabadiliko hayo jana alipokutana na wahariri na waandishi waandamizi wa vyombo mbalimbali vya habari, katika mkutano uliofanyika ofisini kwake Dar es Salaam.

Pinda alisema awali kulikuwa na wilaya 114 lakini baada ya  Rais Kikwete kuanzisha wilaya mpya 19, idadi ya wilaya zote nchini zimefikia 133 na kwamba uteuzi umezingatia idadi hiyo.

“Tunao Ma-DC wapya 70 na ukiangalia katika kundi hili, wamo vijana wenye umri kati ya miaka 30 na 40 hivi na pia mtaona kuwa wamo wabunge wa viti maalumu kama watano hivi, Rais ameamua kuwapa nafasi hizo,”alisema Pinda na kuongeza:

“Pia tumeendelea kutekeleza wazo la kuwa na akina mama wengi kwa hiyo katika orodha nitakayoisoma wapo kama 43, karibu asilimia 30 na kidogo…hivyo kazi hii imechukua muda mrefu kwasababu kulikuwa na masuala haya ya vetting (uhakiki) lakini hatimaye mheshimiwa Rais amekamilisha kazi hiyo”.

Pinda alisema wakuu hao wamepewa siku saba kufika katika vituo vyao vya kazi na kuapishwa na wakuu wa mikoa husika na kwamba baada ya hapo, watashiriki mafunzo ya wiki mbili yatakayofanyika mkoani Dodoma.

Pinda alisema wakuu wa wilaya 51 wa zamani wameachwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo umri mkubwa, ugonjwa pamoja na sababu za kiutendaji.

Walioachwa
Uchambuzi zaidi umebaini kuwa miongoni mwa walioachwa na wilaya zao kwenye mabano ni pamoja na Evans Balama (Mbeya), Zainab Kukwega (Makete), Samwel Kamote (Bukoba), Salum Nyakonji (Ngara) na  Othman Mdoe (Mwanga).

Wengine walioachwa ni Musa Samizi (Moshi), Hawa Mchopa (Ruangwa),Dk  Ian Lengibori (Babati), Winfrid Ligubi (Hanang), Frank Uhaula (Kiteto), Geofrey Ngatuni (Musoma Mjini),   Esther Wakali (Ileje), Gabriel Kimoro (Mbozi) na Kanali  John Mzurikwao (Sumbwanga).

Wengine walioachwa ni Joyce Mgana (Nkansi), Philimon Shelutete (Geita), Zainabu Kondo (Magu), Henry Clemence (Mkuranga), Thomas Ole Sabaya (Songea), Kanali Edmund Mjengwa (Mbinga), Bahati Matala (Kahama) na Grace Mesaki (Iramba).

Pia wamo Florence Horombe (Nzega), Stanley Kolimba (Uyui), Kapteni Seif  Mpembenwe (Handeni) na Rashid Ndaile (Mkinga).

Kwa upande wa nafasi 20 ambazo zilikuwa wazi, uchambuzi wetu umebaini kuwa zilitokana na wakuu wa wilaya tatu kuchaguliwa kuwa wabunge ambao ni Naibu Waziri wa Nchi (Tamisemi – Elimu) Kassim Majaliwa, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba na mtangulizi wake kabla ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Athumani Mfutakamba ambaye pia ni mbunge wa Igalula.

Kwa upande wa wakuu wa wilaya 15 waliopandishwa vyeo kwa kuteuliwa kuwa wakuu wa mikoa ambayo iko kwenye mabano ni John  Tupa (Mara), Saidi Mwambungu (Ruvuma), Chiku Gallawa (Tanga), Leonidas Gama (Kilimanjaro), Dk. Rehema Nchimbi (Dodoma), Elaston Mbwillo  (Manyara)  na Kanali Fabian Massawe (Kagera).

Wengine ni Fatma Mwassa (Tabora),
Ali Rufunga (Shinyanga), Ernest Ndikillo (Mwanza), Magesa Mulongo (Arusha), Dk Rajab Rutengwe (Katavi), Magalula Saidi Magalula (Geita), Paschal Mabiti (Simiyu) na Kapteni Asery Msengi (Njombe).

Nafasi nyingine mbili zilibaki wazi baada ya Nape Nnauye kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wakati aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Cleophace Rugarabamu nafasi yake ilibaki wazi baada ya kufariki dunia.

Walioteuliwa

Waandishi wa habari ambao wameteuliwa kuwa wakuu wa wilaya ni pamoja na aliyekuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Jacqueline Liana na aliyewahi kuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari Ltd, Muhingo Rweyemamu.

Wengine ni Mtangazaji wa zamani wa iliyokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), Ahmed Kipozi, Mtangazaji wa kituo cha Televisheni cha ITV mkoani Arusha, Novatus Makunga na Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji (TBC), Suleiman Mzee.

Kwa upande wa wabunge wa zamani wamo Ponsiano Nyami, Suleiman  Kumchaya, Dk Charles Mlingwa, Manju Msambya, Omar Kwaangw’, Venance Mwamoto, Benson Mpesya, Daudi Felix Ntibenda, Ramadhani Maneno, Gulamhusein Kifu na Esterina Kilasi.

Kadhalika yumo aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Amani Mwenegoha na wabunge wa viti maalum ambao ni Martha Umbula, Rosemary Kirigini na Lucy Mayenga.

No comments:

Post a Comment