SIKU KADHAA BAADA YA JK KUFANYA MABADILIKO KWENYE BARAZA LA MAWAZIRI…IGP MWEMA NAYE ASUKA ‘BARAZA LAKE LA MA-RPC’
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP), Saidi Mwema amefanya mabadiliko
katika jeshi hilo kwa kuwahamisha makamanda wa polisi wa mikoa kadhaa,
kuwateua makamanda mapya na wakuu wa vitengo ndani ya jeshi hilo.
Katika mabadiliko hayo ambayo utekelezaji wake utaanza Juni 1, mwaka
huu, IGP Mwema pia amewateua makamanda wa polisi wa mikoa mipya minne ya
Geita, Njombe, Simiyu na Katavi.
Msemaji Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Advera Senso alisema jana
kuwa mabadiliko hayo ni ya kawaida katika kuimarisha utendaji ndani ya
jeshi hilo, pia kutekeleza maboresho (reforms) yanayoendelea kufanywa.
ASP Senso alisema miongoni mwa maboresho hayo ni kuundwa kwa vikosi
vitatu maalum vitatu vipya vya polisi ambavyo ni Mazingira (Enviromental
Police Unit), Utalii (Tourism Police Unit) na Migodi ya Madini (Mining
Police Unit).
Alisema katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Kamanda
wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP),
Thobias Andengenye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Utawala na Rasilimali,
Polisi Makao Makuu na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa RPC Manyara,
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Liberatus Sabas.
Kamanda wa
Polisi mkoa wa Morogoro, SACP Adolfina Chialo amehamishiwa Makao Makuu
ya Upelelezi (CID – HQ) na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Kamanda
wa Polisi wa mkoa wa Ilala, ACP Fautine Shilogile.
Mabadiliko
mengine yamewagusa RPC Kilimanjaro, SACP Absalom Mwakyoma ambaye
amehamishiwa mkoani Mara akibadilishana na RPC Mara, ACP Robert Boaz
ambaye amehamishiwa mkoa wa Kilimanjaro.
Senso alisema RPC
Ruvuma, SACP Michael Kamuhanda amehamishiwa mkoani Iringa kuchukua
nafasi ya ACP Evarist Mangala ambaye amehamishiwa mkoa wa Shinyanga,
wakati aliyekuwa kamanda wa Shinyanga, ACP Diwani Athumani amehamishiwa
mkoani Mbeya kuendelea na wadhifa wake huo.
Aliyekuwa RPC
Mbeya, ACP Advocate Nyombi amehamishiwa Ofisi ya Upelelezi Makao Makuu
katika kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini huku aliyekuwa Mkuu wa Kikosi
cha Kutuliza Ghasia (FFU), Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP Ferdinand
Mtui akiteuliwa kuwa mkuu wa kikosi hicho nchini, kuchukua nafasi ya
SACP Anaclet Malindisa ambaye anastaafu.
Makamanda wa Polisi
wapya wa mikoa walioteuliwa na mikoa yao kwenye mabano ni aliyekuwa
Ofisa Mnadhimu mkoani Arusha, ACP Akili Mpwapwa (RPC Manyara), aliyekuwa
Ofisa wa Opareshini Mwanza, ACP Philipo Kalangi (RPC Kagera) aliyekuwa
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Arusha, ACP Leonard Paul (RPC
Geita) na aliyekuwa Ofisa Mnadhimu mkoa wa Dodoma, ACP Furgence
Ngonyani (RPC Njombe).
Wengine ni Ofisa wa Oparesheni Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, ACP Marieta Minangi (RPC Ilala), ACP George
Mwakajinga aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Lindi anakuwa RPC Lindi, ACP Linus
Sinzimwa kutoka CID Makao Makuu anakuwa RPC Singida na ACP Salum Msangi
pia kutoka CID Makao Makuu anakuwa RPC Simiyu.
Senso alisema
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Kimataifa Makao Makuu ACP Dhahir
Kidavashari anakuwa RPC Katavi, RCO Mwanza, ACP Deusdedith Nsimike
anakuwa RPC Ruvuma, ACP Saada Juma Haji ambaye ni Ofisa Mnadhimu Ilala
anakuwa Kamanda wa Kikosi cha Reli Dar es Salaamn na Mkuu wa Usalama
Barabarani mkoa wa Arusha, ACP Amir Konja anahamia Dar es Salaam
kuendelea na kazi hiyo.
Walioteuliwa kuwa wakuu wa vikosi vipya
ni ACP George Mayunga kutoka CID Makao Makuu anayekuwa mkuu wa Kikosi
cha Ulinzi wa Mazingira, kikosi cha Ulinzi wa Watalii kitaongozwa na ACP
Benedict Kitarika kutoka Kitengo cha Sheria na Utafiti Makao Makuu na
ACP Deusdedith Katto kutoka Oparesheni Makao Makuu ataongoza Kikosi cha
Ulinzi wa Migodi ya Madini.
Senso alisema mabadiliko hayo pia
yamevigusa vyuo vya polisi ambapo aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Dar es
Salaam, SACP Elice Mapunda ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mafunzo Polisi Makao
Makuu na nafasi yake kuchukukiwa na Mkuu wa Chuo cha Kidatu, ACP Ally
Lugengo.
Mkuu wa Mafunzo katika Chuo cha Polisi Moshi, ACP
Nasser Mwakambonja amehamishiwa Kidatu ambako anakwenda kuwa Mkuu wa
Chuo hicho wakati aliyekuwa Mkuu wa Mafunzo SACP Abdulrahman Kaniki
ameteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Utafiti cha Jeshi hilo.
Senso alisema maofisa wanaotarajiwa kustaafu utumishi wao ni Mkuu wa
Mafunzo wa Kitengo cha Sheria na Utafiti, SACP Donald Kaswende na baadhi
ya makamanda wa polisi wa mikoa.
Makamanda hao na mikoa yao
kwenye mabano ni SACP Henry Salewi (Kagera), ACP Sifueli Shirima (Lindi)
SACP Celina Kaluba (Singida) na Mkuu wa Usalama Barabarani Kada Maalum
ya Dar es Salaam, ACP Vitus Nikata.
No comments:
Post a Comment