Thursday, May 3, 2012

Baraza la Mawaziri laiva


 
IKULU YASEMA RAIS ANASUKA TIMU YA WATU MAKINI KUKATA KIU YA WATANZANIA, WATATANGAZWA WAKATI WOWOTE KUANZIA SASA                                               IKULU imewataka Watanzania watarajie Baraza bora la Mawaziri muda wowote kuanzia leo ambalo limekuwa likisukwa kwa umakini mkubwa na Rais Jakaya Kikwete.Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliliambia gazeti hili jana kuwa: “Rais anasuka Baraza makini la Mawaziri. Yaani kama ni chakula kikiwekwa mezani kila mtu anatakiwa awe na hamu ya kupakua na kula. Kama ni njaa basi itakwisha nadhani muda si  mrefu.”

Balozi Sefue alisema jambo zito kama mabadiliko ya mawaziri, linahitaji umakini wa hali ya juu hivyo Watanzania wanapaswa kumpa muda Rais kusuka baraza bora linaloweza kuwa chachu ya ufanisi katika utendaji kazi wa Serikali.

“Nadhani, jambo la msingi tumpe muda Mheshimiwa Rais afanye uteuzi wa watu bora. Naamini kiu hiyo itakatwa muda mfupi ujao wala sidhani kama itachukua muda mrefu sana. Watanzania wajiandae kupata baraza bora,” alisema.

Balozi Sefue alisema Rais Kikwete anajua Watanzania wana kiu ya kupata Baraza jipya la Mawaziri lakini akasema mkuu wa nchi anachokifanya sasa ni kuhakikisha kiu hiyo inakatwa kwa kuwapa wananchi baraza bora.

Alisema haki itatendeka katika suala hilo kwa kuwawajibisha wanaopaswa kuwajibishwa kadri Rais mwenyewe atakavyokuwa amejiridhisha kwa tuhuma zinazowakabili.

Aliongeza kwamba Rais atafanya uamuzi huo kwa kuangalia matakwa ya Watanzania na aina ya mawaziri ambao taifa linawahitaji kwa sasa.

Balozi Sefue alipoulizwa kwa nini Ikulu haikutoa agizo kwa mawaziri hao kujiuzulu kabla ya Rais kuchukua hatua, alisema uwajibikaji wa namna hiyo ungekuwa ni sawa na kuwalazimisha kitu ambacho siyo kizuri kwani kila mtu alipaswa kujipima mwenyewe.

“Sasa ukimwambia mtu aandike barua ya kujiuzulu maana yake unamlazimisha. Jambo hili la uwajibikaji siyo la kulazimishwa ni mtu mwenyewe anapaswa kujipima na kuchukua hatua. Lakini, ukimwambia aandike barua ya kujiuzulu hata akijiuzulu haijengi dhana nzuri ya uwajibikaji,” alisema.

Alisema suala la uwajibikaji linahitaji dhamira na utashi binafsi na kuongeza, kama mambo hayo yamekosekana kumlazimisha mtu inakuwa bado haijasaidia katika kujenga dhana nzima ya uwajibikaji kama ambavyo imezoeleka.

Kauli ya Rais juzi

Akihutubia katika sherehe za Mei Mosi, zilizofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga juzi, Rais Kikwete alisema amesema amefurahishwa na mjadala mkali ulioibuka bungeni baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Ripoti tatu za Kamati za Bunge za mwaka 2009/10 kuwasilishwa kwa wabunge na kupendekeza kuwajibishwa kwa baadhi ya watendaji serikalini wakiwamo mawaziri wanane.

“Sikukasirishwa na wala kufedheheka na mjadala ule, nilifurahia ripoti kujadiliwa kwa uwazi. Tatizo watu wanasahau mapema. Mimi ndiye niliyeamua ripoti hii ya CAG ijadiliwe kwa uwazi bungeni tangu mwaka 2007. Nilifikia uamuzi huo baada ya kuona wapo baadhi ya watu ambao ni mchwa wanaokula fedha za umma.”

“Kwa hiyo, mjadala ule ulipokuwa unaendelea bungeni nikaona sasa tunaelekea kufanikiwa katika kujenga nidhamu ya matumizi ya  fedha za serikali.... mjadala ulikuwa ni mkali kweli bungeni. Wengi wakitaka mawaziri waliotajwa kwenye ripoti hiyo wawajibishwe. Ninachowaahidi ni kwamba tumejipanga vizuri kutekeleza mapendekezo ya wabunge na Kamati za Bunge.”

Kamati Kuu (CC) ya CCM imeshabariki uamuzi wa Rais kulisuka upya Baraza la Mawaziri. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibu akisema Kamati hiyo imepokea taarifa ya jinsi Rais alivyopanga kuchukua hatua za kuwawajibisha mawaziri na watendaji serikalini na viongozi wa mashirika ya umma waliobainika kuhusika na ubadhirifu ulioainishwa na CAG, Kamati za kudumu za Bunge na wabunge.

“Kamati Kuu inatambua na kuheshimu haki na wajibu wa wabunge kujadili utendaji wa Serikali yao. Inapongeza juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inajadiliwa kwa uwazi na hivyo kuibua upungufu uliojadiliwa,” alisema Nape na kuongeza:

“Kamati Kuu imesisitiza utekelezaji wa uamuzi huo wa Rais ufanywe mapema iwezekanavyo.”
Mawaziri waliotajwa katika ripoti hiyo ya CAG ni William Ngeleja (Nishati na Madini) Omari Nundu (Uchukuzi), Mustafa Mkulo (Fedha), George Mkuchika (Tamisemi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Waziri wa Viwanda na Biashara). CHANZO MWANANCHI COMMUNICATION

No comments:

Post a Comment