Sunday, April 22, 2012

Jahazi la CCM lazidi kuzama



UPEPO wa wanachama wa CCM kujiunga na Chadema umezidi kushika kasi baada ya viongozi zaidi wa chama hicho na mamia wanachama kuhamia Chadema.  Viongozi wa CCM waliohamia Chadema  ni Wilaya ya Monduli, Wilaya za Sengerema, na Kikundi cha Kwaya cha Uhamasishaji wa chama hicho Wilaya ya Magu na mamia ya wachama kutoka katika maeneo hayo.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Monduli, Amani Ole Selenga amesema chama chake kimepokea jumla ya wanachama 300 wa CCM katika kata mbili za Makuyuni na Mto wa mbu wilayani Monduli.

Aliongeza kuwa wengi wa wanachama hao ni wajumbe wa serikali za vijiji na wajumbe wa nyumba kumi.
Kwa mujibu wa Ole Selenga, taarifa za wanachama hao kukimbilia Chadema zilimshtua Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na kudai kuwa mbunge huyo alipanga kurejea jimboni kuzima moto huo.
Mkoa wa Mwanza Katika hatua nyingine zaidi ya wanachama 95 wa CCM kutoka Wilaya za Magu na Sengerema wamerudisha kadi za CCM na kujiunga na Chadema jana.
Wanachama hao ambao kati yao, 45 ni wanakwaya maarufu ya uhamasishaji ya Ngómbe ya Magu ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitumiwa katika kampeni kuhamasisha wananchi kuchagua CCM.
Akitangaza kujiunga wanakwaya hao, Katibu wa Chadema Magu, Bahati Simon alisema jana kuwa wamechukua uamuzi huo baada ya kuona CCM haijawaletea maendeleo wananchi wala wao wenyewe.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana mjini Sengerema na kuhutubiwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa, wanachama 50 wa CCM walihama na kujiunga na Chadema.
Katika mkutano huo, diwani wa CCM Kata ya Lugata kutoka Wilaya ya Sengerema Adrian Tizeba, alitangaza kujiunga na Chadema.  Diwani huyo ambaye ni ndugu wa Mbunge wa Buchosa (CCM), Dk Charles Tizeba, alisema ameamua kuhamia Chadema kwa hiari yake mwenyewe  Diwani mwingine aliyehama CCM na kuingia Chadema ni Hamis Mwagao wa Kata ya Nyampulukano ambaye pia  Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya UVCCM, Wilaya ya Sengerema John Tungu.   Viongozi CCM Arusha waita Dar
Wakati hali ikiendelea kuwa tete, ndani ya CCM viongozi wa ngazi ya juu wa CCM Mkoa wa Arusha wameitwa makao makuu ya chama jijini Dar kueleza kinachoendelea mkoani humo.   Habari za uhakika kutoka ndani ya viongozi wa CCM, zimeeleza kuwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Abdalah Mpokwa na Katibu wa Itikadi mkoani humo, Loota Sanare  Jumatano wiki hii, waliitwa ghafla makao makuu ya CCM na walitarajia kurejea jana jioni kwa ndege.  “Ni kweli kuna viongozi wameitwa haraka Dar es Salaam nadhani wametakiwa  ili kueleza kinachotokea Arusha,” alisema Kiongozi mmoja wa CCM ambaye jina lake linahifadhiwa.  Wakati viongozi hao wakiwa wameitwa Dar es Salaam, viongozi wengine wa CCM wa ngazi ya mkoa na wilaya, kuanzia juzi walikuwa katika wilaya za Ngorongoro katika kata za Enduleni, Longido na Monduli kufuatilia taarifa za viongozi na wanachama wao kuhamia Chadema.  Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Mkoa wa Arusha, Sanare alikiri jana kuwa alikwenda jijini Dar es Salaam ghafla muda mfupi baada ya kurejea safari yake binafsi Nairobi, Kenya. Hata hivyo alikanusha kuitwa na viongozi wa juu wa CCM.  “Ni kweli nipo Dar es Salaam, lakini sipo kwa mambo ya CCM nina mambo yangu, haya mambo ya kuhama watu ni haki yao ila vyombo vya habari mnayakuza sana,” alisema Sanare.   Diwani wa CCM Kata ya Endeleni, James Moringe alikiri kwenda katika Kata hiyo, lakini alikanusha taarifa za kuhama kwa viongozi wa CCM wa kata hiyo na kujiunga na Chadema.  “Wapo viongozi huko, lakini wengi wa hawa wanaodaiwa kuhamia Chadema sio viongozi wa CCM na kuhama kwao kunatokana na mgogoro katika moja ya vijiji katika kata hiyo,” alisema Moringe.  Katika Wilaya za Monduli na Longido pia, viongozi wa chama hicho, wamekuwa wakihaha na kukutana na baadhi ya viongozi wakiwasihi kutokihama chama hicho.  “Tunasumbuliwa sana na taarifa za kuondoka mimi nimeamua kurudi kwanza kijijini kutulia kwani sasa hivi ni sawa na vitisho, lakini kuondoka kupo palepale wakati ukifika,” alisema kiongozi mmoja wa UVCCM wilaya ya Monduli.   Naye Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Monduli, Julias Kalanga ambaye jana alitangaza angekutana na wanahabari pamoja na viongozi na wana CCM wengine kutoa msimamo wao,  hakupatikana na muda wote simu zake za mkononi zilikuwa zimefungwa.  Taarifa ambazo Mwananchi Jumapili inazo ni kwamba Kalanga amekuwa akibembelezwa na viongozi wa juu wa CCM kutotangaza kukihama chama hicho, wakati madai yao UVCCM Mkoa wa Arusha yakifanyia kazi.  Mmoja wa viongozi wa CCM katika wilaya hiyo, alisema kutojitokeza jana kutangaza kukihama chama hicho, kunatokana na kutafakari maombi ya kutofanya hivyo pamoja na hali ya kisiasa nchini ilivyo sasa.  “Watu wote wanafuatilia bunge kujua hatma ya Serikali ya CCM na hasa kutimuliwa kwa mawaziri  sasa tumeona tusubiri kidogo kitakachotokea Dodoma ila msimamo wetu upo palepale,” alisema kiongozi mwingine wa CCM.  Dk Slaa
Akihutubia mkutano wa hadhara mkoani Mwanza, Dk Slaa aliwashukia wabunge wa CCM wanaodai ni wapambanaji wa ufisadi kuwa hawana nia ya dhati kwa vile  wanaogopa wimbi la wanachama kukihama chama chao.  Dk Slaa alisema kama kweli wabunge hao wanaojipambanua kama wapambanaji na ufisadi wangekuwa wangejiunga na Chadema tangu mwaka 2007.
 Dk Slaa alisema chama chake kitafungua kesi wiki ijayo kuishtaki Serikali mahakamani kwa makosa ya uvunjaji wa haki za msingi za binadamu.  Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara wa Uwanja wa Magereza, Dk Slaa alisema chama hicho kimeamua kufanya hivyo ili kukomesha unyanyasaji na kuwataka wananchi na viongozi wote ambao wamekuwa wakibambikiwa kesi kukusanya taarifa zote ambazo zitakuwa sehemu ya ushahidi wa mashtaka hayo ili mchakato huo ukamilike.  Imeandikwa na Claud Mshana, Frederick Katulanda, Geita, Mussa Juma, Peter Saramba, Arusha

No comments:

Post a Comment