Wednesday, April 18, 2012

Millya kupewa kadi ya Chadema kijijini kwao







                                                                                                                                                                                                                                                                                             SIKU kadhaa baada ya aliyekuwa   Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Arusha, James ole Millya kutangaza kujiuzulu nafasi zake zote ndani ya chama hicho na kuhamia Chadema, chama hicho cha upinzani kimemwandalia utaratibu maalumu kwa kushirikiana na wananchi ili kumkabidhi kadi ya uanachama kijijini kwao.

Akizungumza na gazeti hili jana mkoani hapa, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema kwa sasa viongozi Mkoa wa Arusha, wanafanya mawasiliano na viongozi wa chama hicho kutoka Mkoa wa Manyara na wilayani Simanjiro, juu ya kuweka mazingira ya kumpatia kadi hiyo ndani ya wiki hii.

Alisema Millya mwenyewe anapenda kukabidhiwa kadi hiyo katika kijiji alikozaliwa, Naisinyai wilayani Simanjiro, huku wenyeji wake wakishuhudia tendo hilo.

Golugwa alisema lengo la kutaka kukabidhiwa kadi kijijini alikozaliwa, Millya amelichagua kutoka moyoni mwake na amekuwa akitamani kupewa kadi huku ndugu, jamaa na marafiki, washuhudie.

Alisema chama hicho kimeona ni vema wakasaidiana na wenzao Simanjiro na Manyara kuandaa hafla ya kumkabidhi kadi huku wananchi wakishuhudia tendo hili.

Aidha, aliwaondoa wasiwasi wanachama na wakazi wa Arusha na Tanzania, kuhusu kupokea wanachama wa CCM, kuwa waondoe hofu sababu chama kipo makini na kimejiandaa kwa kila mapambano.

Alisema hata siku moja katika ngome yao hataweza kupenya mamluki au fisadi yoyote na kukivuruga chama, sababu ngoma hiyo wanaicheza wenyewe na utaratibu wa uongozi ndani ya chama upo wazi mtu hapewi uongozi, na ni lazima achunguzwe kwa muda mrefu na kukubalika na wanachama wote.

Naye Mjumbe wa Baraza la UVCCM na Mwenyekiti wa Umoja huyo wilayani Arumeru, Kennedy Mpumilwa, alisema Millya ametumia haki yake kikatiba kwenda chama anachopenda.

Millya aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa tangu mwaka 2008, alijiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya CCM na kuhamia Chadema juzi, huku akikishutumu chama hicho tawala kwa kukosa uwazi.

No comments:

Post a Comment