Sunday, April 22, 2012

*WAWILI WAGOMA KUWASILISHA BARUA , PINDA KUTOA TAMKO KESHO



Na Waandishi Wetu,Dodoma
WAKATI kishindo cha shinikizo la kutakiwa kujiuzulu mawaziri nane wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kikizidi kurindima, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali itatoa tamko lake rasmi kesho.

Awali Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenister Mhagama aliwaambia waandishi wa habari juzi usiku kuwa chama hicho kimefanya maamuzi magumu ambayo yangetangazwa na Pinda mjini hapa jana.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda alipoombwa na waandishi wa habari jana kuzungumzia sakata hilo, hakukanusha wala kukiri kuwapo kwa azimio hilo zaidi ya kusema wananchi wasubiri hadi kesho atakapotoa taarifa rasmi.
Alipoulizwa kama kuna mawaziri ambao wameshawasilisha barua zao za kujiuzulu hadi kufikia jana mchana, Pinda alijibu kwa kifupi kuwa ‘bado hatujapokea, lakini kama wapo watatuletea tu”.
Ingawa Waziri Mkuu hakukiri kupokea barua yoyote, taarifa zisizo rasmi, zilisema mawaziri watano waliokumbwa na msukosuko huo wamekabidhi barua zao huku Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami akikataa kufanya hivyo.

Mwingine ambaye anatajwa kuwa hajawasilisha barua yake, ni Waziri wa Fedha Mustapha Mkulo ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi.
Chami ajitetea

Dk. Cyril Chami amesema hataandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo na kusema anawaachia wananchi wapime kama kweli anastahili kujiuzulu ama la.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana alisema yuko tayari kujiuzulu endapo tu wananchi na wabunge  watampa fursa ya kusikiliza utetezi wake na kama bado wataona ana makosa,yuko tayari kuachia ngazi.
Dk Chami ni mmoja wa mawaziri ambao Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kikao cha Wabunge wa chama hicho, kimewapa muda hadi kufikia kesho wawe wameandika barua za kujiuzulu.
Kiini cha D. Chami kutakiwa kujiuzulu, ni kauli za Wabunge wa CCM kuwa anamkingia kifua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango nchini (TBS), Charles Ekelege anayetuhumiwa kwa ufisadi.
Hata hivyo Dk Chami alisema hadi jana wizara yake ilikuwa haijapatiwa ripoti ya Mamati Maalumu ya Bunge ya Mashirika ya umma iliyokwenda kumchunguza Ekelege katika nchi za Hongkong na Singapore.
“Nataka wananchi wanielewe nitamwajibishaje Ekelege wakati ripoti ya kamati teule ya Bunge iliyomchunguza mimi sina…ningejengaje hoja kwa Rais bila kuwa na tuhuma zake?”alihoji D. Chami.
Alisema Mkurugenzi wa TBS ni mteule wa Rais na kuna taratibu zake ambapo taarifa ya kamati hiyo ndiyo ingeisadia Bodi ya Wakurugenzi ya TBS kumjadili na kupitisha maamuzi,”alisema.
Alifafanua hata ripoti maalumu ya ukaguzi iliyofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hawakuwa wamepewa na wamepatiwa siku tatu zilizopita mjini Dodoma.
“Bado najiuliza CAG alikuwa na agenda gani na wizara yangu kwa sababu hakutupa ripoti yake lakini akawapa baadhi ya wabunge mpaka tulipofuatulia juzi baada ya kelele za wabunge”alisema.
Aliongeza kusema Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo, leo anashutumiwa kwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma(CHC) bila kufuata utaratibu.
“Utashangaa leo Mkulo anashutumiwa kwa kutofuata taratibu kumsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa CHC lakini leo mimi nashinikizwa nimsimamishe kazi Mkurugenzi wa TBS bila kufuata taratibu,”alisema.
Dk Chami alisema amejitahidi kuomba taarifa hiyo ya Kamati Teule iliyomchunguza Ekelege lakini hadi jana hajapatiwa zaidi ya kuambiwa ilipelekwa kwa Spika na hajaambiwa baada ya hapo ilikwenda wapi.
Hata hivyo habari za uhakika ambazo gazeti hili inazo , zinaonyesha kuwa baada ya ripoti hiyo ya kamati kufika kwa Spika, Spika naye aliipeleka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Katika kuthibitisha Wizara ya Viwanda na Biashara haikuwa imeipata barua hiyo, Februari 2,2012 Katibu Mkuu, Joyce Mapunjo alimwandikia barua Katibu wa Bunge akimkumbusha awapatie ripoti hiyo.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba GA96/352/01 iliyopelekwa kwa Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashilila, ilisema”nimeona nikukumbushe unisaidie ripoti hiyo niweze kutekeleza maagizo ya kamati”.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Februari 10,2012 Kamati za PAC na POAC na ile ya Viwanda na Biashara zilikutana Dodoma ambapo Kamati iliendelea kumtuhumu Mtendaji Mkuu wa TBS.
Katika kikao hicho, wizara iliagizwa kuwasilisha kwa CAG ripoti ya idadi ya magari yaliyokaguliwa na mapato yake, na wizara ikakabidhi ripoti hizo  Februari 15,2012 kwa barua yenye kumb GA.96/352/01.
Ni kwa maelezo hayo, Dk. Chami alidai tangu wakati huo ofisi yake haijawahi kupokea ripoti nyingine yoyote iwe ya CAG au kutoka kwa Spika zaidi ya kufahamu kuwapo kwake bungeni wiki hii.
Dk Chami alifafanua kuwa kukosekana kwa ripoti hizo kulimfanya afungwe mikono ya kwenda kwa Rais kumshauri amuondoe Ekelege kwa kuwa hakuwa na ripoti iliyokuwa ikionyesha tuhuma zake.
Kutokana na msingi huo, Dk. Chami alisema chombo alichobakia nacho kuchukua maamuzi ni Bodi ya Wakurugenzi ya TBS na bodi hiyo iliundwa na kuzinduliwa Machi 29, 2012.
Dk Chami alisema bodi hiyo ilikutana Aprili 5,2012 na Wizara yake ikapokea ushauri wa Bodi hiyo Machi 19,2012 na wakati ripoti ya ukaguzi maalumu wa CAG akiipokea Aprili 18 akiwa Bungeni Dodoma.

 


Omari Nundu
Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi,Omari Nundu jana alitumia Bunge kurusha kombora kwa Kamati ya Mindombinu kuwa imekuwa na taarifa zisizo sahihi.
Nundu alisema taarifa zote juu yake ni za uongo huku akikanusha kwamba hajawahi kusaini makubaliano (MoU) yoyote kuhusu mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam gati  namba 13 na 14.

Ngeleja
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, alipoulizwa na mwandishi wetu kupitia ujumbe mfupi wa maandishi(SMS) alijibu kwa kifupi ‘Tuziachie mamlaka za maamuzi”.
Mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu ili kuinusuru Serikali ni Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo,Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.
Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu.
Taarifa zilizopatikana juzi usiku zilieleza kuwa katika kikao hicho, mawaziri hao kwa pamoja waliwekwa katika eneo maalumu na wakawa wakiitwa mmoja mmoja kwa ajili ya mahojiano na wabunge na baadaye kupewa msimamo wa chama.
Baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Waziri Mkuu akaendesha kikao kingine cha faragha, safari hii kikimhusisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Frederick Werema na Waziri William Lukuvi.

Wengine walioitwa katika kikao hicho ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, Mwigulu Mchemba,Katibu wa Oganaizesheni na Mahusiano ya Nje Januari Makamba na Katibu wa wabunge wa chama hicho, Jenister Mhagama.

Hata hivyo mwenye mamlaka ya kuwafukuza Mawaziri kwa mujibu wa Katiba ni Rais Jakaya Kikwete aliyewateua ingawa hata hivyo badhi ya wabunge wanamtuhumu Rais kuwa si mtu wa kufanya maamuzi haraka na kwa shinikizo.

Jana baadhi ya mawaziri wanaotakiwa kuachia ngazi waliingia katika ukumbi wa Bunge na kukalia viti vyao lakini mara baada ya kuahirishwa kwa kikao, waliondoka haraka katika viwanja vya Bunge.

Baadhi yao walipotafutwa  kwa simu ili watoe ufafanuzi na msimamo wao kuhusiana na azimio hilo la CCM, ama simu zao zilikuwa hazipatikani kabisa na zingine hazikupokelewa, zilikatwa.

Zitto aendelea kutafuta saini

Katika hatua nyingine,Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema hoja ya kumpigia Waziri Mkuu kura ya kutokuwa na imani ipo pale pale kama mawaziri wanaotajwa kwa ufisadi hawatajiuzulu kufikia kesho.
“Sisi tunasema bila kumwajibisha Waziri Mkuu hawa mawaziri waliotajwa hawatatoka na wasipotoka madudu haya yatarudia…kwa hiyo ni wao mawaziri kupima na kuwajibika au wamweke reheni Waziri Mkuu,”alisema.
Mbunge huyo alirejea wito wake wa kuwaomba wabunge wenye uchungu na ubadhirifu na ufisadi waunge mkono utiaji wa saini hizo na kwamba kama mawaziri watajiuzulu ifikapo Jumatatu, wataondoa hoja hiyo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Kambi rasmi ya upizania Bungeni, Freeman Mbowe alirejea msimamo wake wa kuomba kufanyiwa mabadiliko ya katiba ya nchi na kanuni za Bunge ili Spika asiwe anatokana na chama chochote cha siasa.
Mbowe alitoa kauli hiyo kutokana na kile alichodai,  hatua ya Spika Anne Makinda kutafsiri vibaya kanuni za Bunge na Katiba ya nchi ili tu kuilinda Serikali na Waziri Mkuu wake ili asipigiwe kura ya kutokuwa na imani.
“Mambo ya ajabu sana eti Spika anasema hili zoezi letu ni batili…sisi tunamshangaa, wanasheria wanamshangaa na hata wananchi wanamshangaa… anatoleaje mwongozo kwa kitu ambacho hakipo mezani kwake?”alihoji.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema kanuni inataka ili hoja ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Waziri mkuu iweze kufikishwa ofisi ya Spika, ni lazima ipate sahihi za wabunge 70 na ndicho wanachokifanya.

Wasomi wazungumza

Baadhi ya wasomi wa Chuo Kikuu wamelitaka Bunge kufuata sheria na kanuni za Bunge kabla ya kufanya maamuzi hayo kwa sababu mawaziri hao wanaripoti kwa Rais Jakaya Kikwete na si Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, wasomi hao walisema kuwa, kutokana na hali hiyo wabunge hao wanapaswa kufuata kanuni ili waweze kutambua kuwa mwenye mamlaka ya kuwaondoa mawaziri hao ni  Rais na si Waziri Mkuu, hivyo basi kumlazimisha aondoke madarakani ni sawa na kumuonea.

“Mimi naona wanamuonea bure Waziri Mkuu Pinda, kwa sababu hana mamlaka ya kuwaondoa Mawaziri madarakani badala yake wanatakiwa kuangalia kanuni kwanza ndipo waweze kufanya maamuzi,”alisema Profesa Simon Mbilinyi mwasiasa mstaafu nchini.

Aliongeza kutokana  na hali hiyo wabunge hao walipaswa kumuandikia barua Rais Kikwete na kumtaarifu kuwa mawaziri wake wameshindwa kufanya kazi badala yake wanatakiwa kuwajibika kulingana na makosa waliyofanya.

Alisema kutokana na hali hiyo maamuzi ambayo yangeweza kutolewa na rais yangekuwa sahihi kwa sababu yamefuata sheria na taratibu zilizotungwa na Bunge.

Alisema kitendo cha wabunge hao kumshinikiza Waziri Mkuu kujiuzulu au kuwaondoa mawaziri hao ni kinyume na sheria na ni sawa na kumuonea, jambo ambalo linaweza kumfanya afanye maamuzi bila ya kufuata taratibu.

Hata hivyo, Profesa Abdalah Safari alisema kuwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) ni wanafiki, na kwamba wanashindwa kufanya maamuzi mpaka wasubiri nguvu kutoka kwa wapinzani.

Alisema kutokana na hali hiyo wabunge hao wamepoteza mwelekeo na kwamba wamejaa woga jambo ambalo limesababisha kuendekeza ufujaji wa mali za umma kwa makusudi.

Naye Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Matakatifu Agustino cha Mwanza (Sauti) Dk  Charles Kitima amesema  mchakato unaofanywa na wabunge kwa   lengo la kumg’oa Waziri Mkuu Pinda sio suluhu ya kutibu tatizo la uwajibikaji kwa viongozi  serikalini.

 “Tunalia watu wajiuzulu wakati tumebaki na mfumo ambao unaruhusu siasa chafu, Mahakama inaingiliwa katika maamuzi yake Tume ya Uchaguzi haiko huru, hili haliwezi kuleta mabadiliko sababu Rais atateua mtu mwingine kufanya kazi hiyo na shughuli zitaendelea kama kawaida”alisema Dk Kitima.

Dk Kitima ambaye alikuwa akichangia  mada  katika kipindi cha jicho letu katika habari kinachorushwa na kituo cha Televisioni cha Star Tv cha jijini Mwanza jana, alisema njia pekee ambayo inaweza kuleta  mabadiliko ni kubadilisha mfumo utakaowezesha viongozi kuwajibika kwa wananchi.

“Walijiuzulu Edward Lowasa, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha nini kimebadilika, rais ameteua wengine matatizo bado yanaendelea serikalini tatizo si watu bali mfumo uliopo ambao unatoa fursa kwa viongozi na watendaji kuwajibika kwa waliowateua”alisema Dk Kitima.

Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema na Habel Chidawali, Dodoma, Patricia Kimelemeta, Geofrye Nyang’oro

Orodha ya wabunge waliosaini:
      
  1. 2.     Rashid Ali Abdallah – CUF
  2. 3.    Chiku Aflah Abwao- Chadema
  3. 4.     Saluim Ali Mbarouk – CUF
  4. 5.    Salum Khalfam Barwany –  CUF
  5. 6.     Deo Haule  Filikuchombe- CCM
  6. 7.    Pauline Philipo Gekul- Chadema
  7. 8.    Asaa Othman  Hamad- CUF
  8. 9.     Prof.Kuliyokela Kahigi- Chadema
  9. 10.    Naomi  Mwakyoma Kaihula – Chadema
  10. 11.     Sylvester Kasulumbayi- Chadema
  11. 12.     Raya Ibrahim Khamis  - Chadema
  12. 13.     Mkiwa Hamad Kiwanga  -  CUF
  13. 14.     Susan  Limbweni Kiwanga- Chadema
  14. 15.     Grace Sindato Kiwelu –Chadema
  15. 16.     Kombo Khamis Kombo – cuf
  16. 17.     Joshua  Samwel  Nassari – Chadema
  17. 18.     Tundu Antiphas Lissu- Chadema
  18. 19.     Aphaxar  Kangi Lugola- CCM
  19. 20.    Susan Anselim Lymo- Chadema
  20. 21.     Moses Machali – NCCR Mageuzi
  21. 22.     John Shibuda Magalle – Chadema
  22. 23.    Faki  Haji  Makame-  CUF
  23. 24.     Esther Nicholas Matiko- Chadema
  24. 25.     Joseph Osmund Mbilinyi- Chadema
  25. 26.    Freman  Aikaeli Mbowe- Chadema
  26. 27.    Kurudhum Jumanne Mchuchuli – Chadema
  27. 28.     Halima James Mdee-Chadema
  28. 29.    John John Mnyika- Chadema
  29. 30.     Augustino Lyatonga Mrema- TLP
  30. 31.     Maryam Salum  Msabaha- Chadema
  31. 32.     Peter Msingwa-chadema
  32. 33.    Christowaja Gerson Mtinda- Chadema
  33. 34.     Philipa Geofrey Mturano- Chadema
  34. 35.    Christina Lissu Mughwai- Chadema
  35. 36.    Joyce John  Mukya – Chadema
  36. 37.    Mchungaji  Israel  Yohane  Natse – Chadema
  37. 38.    Philemon Ndesamburo- Chadema
  38. 39.     Ahmed  Juma Ngwali-  CUF
  39. 40.    Vincent  Josephat  Nyerere- Chadema
  40. 41.     Rashid  Ali Omar-  CUF
  41. 42.    Meshack  Jeremiah Opulukwa- Chadema
  42. 43.     Lucy Philemon Owenya- Chadema
  43. 44.     Rachel Mashishanga- Chadema
  44. 45.     Mhonga Said Ruhwanya – Chadema
  45. 46.     Conchesta Rwamlaza – Chadema
  46. 47.    Moza Abedi  Saidy-  CUF
  47. 48.    Joseph  Roman Selasini – Chadema
  48. 49.     David Ernest  Silinde- Chadema
  49. 50.     Rose Kamili Sukum  - Chadema
  50. 51.     Cecilia Daniel Paresso- chadema
  51. 52.    Kabwe Zuberi Zitto- Kigoma Kaskazini
  52. 53.     Magdalena Sakaya –  CUF
  53. 54.     Rebecca Mngodo-  CUF
  54. 55.     Sabreena Sungura -Chadema
  55. 56.    Hamad Rashid Mohammed- CUF
  56. 57.    Rukia Kassim Ahmed- CUF
  57. 58.    Mustapha Boay Akoonay -Chadema
  58. 59.     Abdalla Haji Ali -CUF
  59. 60.    Khatibu Said Ali -CUF
  60. 61.     Hamad Ali Hamad -CUF
  61. 62.      Riziki Omar Juma -CUF
  62. 63.     Haji Khatibu  Kai -CUF
  63. 64.     Anna Marystella John Malack -Chadema
  64. 65.     Hamad Rashid Mohamed  -CUF
  65. 66.     Rajab Mbarouk Mohamed -CUF
  66. 67.     Thuwayba Idrissa Muhamed -CUF
  67. 68.      Masoud Abdallah Salum -CUF
  68. 69.     Muhamad Ibrahim Sanya -CUF
  69. 70.     Ali Khamis Seif -CUF
  70. 71.     Haroub Muhammed Shamis -CUF
  71. 72.     Amina Amour Nassoro -CUF

No comments:

Post a Comment