Friday, 13 April 2012 20:57
VIKOSI vya askari nchini Guinea Bissau vimefanya mapinduzi ya
Serikali nchini humo jana, kwa kuzingira makazi ya Waziri Mkuu wa nchi
hiyo, makao makuu ya chama tawala na kushikilia redio na televisheni za
Serikali.
Vikosi hivyo vimefanya mapinduzi hayo huku nchi hiyo
ikitarajiwa kufanya uchaguzi wa marudio Aprili 29, baada ya awamu ya
kwanza ya uchaguzi wa Machi 18 kushindwa kutoa mshindi wa jumla wa kura
za urais.
Askari hao walivamia makazi ya Waziri Mkuu anayemaliza
muda wake, Carlos Gomes Junior ambaye anaongoza katika awamu ya kwanza
ya uchaguzi wa rais, huku mwenyewe akiwa hajulikani aliko.
Katika
uchaguzi huo wa Machi 18, Gomes ambaye alikuwa akiwania nafasi hiyo kwa
tiketi ya chama tawala alishinda kwa asilimia 48.9 na mpinzani wake
mkuu, Kumba Yala akipata asilimia 23.26 ya kura zote.
Wanajeshi
hao wamezingira na kushikilia vituo vyote muhimu vya mawasiliano jana,
siku moja kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi wa marudio
zilizotarajiwa kuanza leo na kumalizika Aprili 21.
Wapinzani
walionya kwamba hakuna sababu ya kufanya kampeni mapema jana, huku
wakionya kwa yeyote atakayekaidi agizo hilo, lakini muda mfupi baadaye
nchi hiyo ilitikiswa na taarifa za mapinduzi ya kijeshi.
Tangu
kupata uhuru wake kwa nguvu za kijeshi mwaka 1974, jeshi na Serikali ya
nchi hiyo vimekuwa katika nguvu inayoelekeana na muda mwingine mivutano,
hivyo kufanya nchi hiyo isiwe Rais aliyemaliza muda wake.
Milio
ya risasi na mabomu ya kurushwa kwa mikono iliosikika katika mitaa
mbalimbali kwenye mji mkuu wa nchi hiyo alfajiri ya kuamkia jana, huku
ikizua hofu kubwa katika nchi hiyo ambayo iko katika kipindi cha
kuelekea marudio ya uchaguzi mkuu.
“Tulishambuliwa kwa risasi na
mabomu, tuloilazimika kujibu mapigo,” alisema mmoja wa maofisa wa polisi
aliokuwa lindo katika makazi ya Gomes, akifafanua kuwa awali kiongozi
huyo alikuwemo katika makazi hayo, lakini alifanikiwa kutoroka.
Moja
ya vyanzo vya kijeshi kilikaririwa na AFP kikieleza kwamba wanamtafuta
kwa juhudi zote Gomes bila kujali alikojificha na kwamba wana uhakika wa
kumtia nguvuni.
Taarifa hizo zilieleza kwamba askari walitanda
katika maeneo mengi ya mji uliogubikwa na giza usiku wa kuamkia jana,
huku umeme ukiwa umekatwa na raia wakiwa wamejihifadhi majumbani mwao.
Awali,
wanajeshi walishikilia jengo la makao makuu ya chama tawala cha nchi
hiyo ambako vikosi zaidi ya 20 vimetapakaa katika eneo hilo na kuzuia
matangazo ya redio na televisheni.
Vikosi hivyo pia vililizingira
jingo la Ikulu ya Rais wan chi hiyo huku Rais anayemaliza muda wake
akisimamia kipindi cha mpito, Raimundo Pereira akiwa hajulikani aliko.
Kumekuwa
na mashaka ya kuibuka kwa vurugu katika uchaguzi wa marudio
unaotarajiwa kufanyika kwenye taifa hilo masikini ambalo limekuwa
likitawaliwa na vurugu za kisiasa, pia kujulikana kuwa miongoni mwa
mataifa yanayopitisha madawa ya kulevya kati ya Amerika ya Kusini na
Ulaya.
Upinzani nchini humo ukiongozwa na mgombea aliyeshika
nafasi ya pili katika uchaguzi wa awali mwezi Machi mwaka huu, Kumba
Yala, Rais wa zamani ambaye anadai kuwa mshindi katika awamu ya kwanza
umetishia kugomea uchaguzi wa marudio Aprili 29 kwa madai kuwa kulikuwa
na udanganyifu katika awamu ya kwanza.
Wagombea wakuu wa upinzani
katika uchaguzi huo akiwemo Yala walisema jana kwamba hatua ya kugomea
uchaguzi wa marudio itakuwa katika msingi wa kusimamia “haki”.
Uapinzani
kwa pamoja ulipiga marufuku kushiriki katika kampeni zozote kuelekea
uchaguzi wa marudio, huku Yala akionya kwamba “Yeyote atakayefanya
kampeni atabeba jukumu la kile kitakachotokea”.
No comments:
Post a Comment