Mkuu wa wilaya Mbozi aliyeachia ngazi Gabriel Kimoro
--
Katika
kile kinachoonyesha uwepo wa mpasuko baina ya watendaji wa kiserikali,
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, Gabriel Kimolo, amejiuzulu
wadhifa wake huo huku akitupa lawama kwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe kuwa sababu ya yeye
kujiweka kando na uongozi wilayani hapo.
Profesa
Maghembe, alikuwa akiongoza Wizara hiyo hadi leo mchana alipotangazwa
kuhamishiwa Wizara ya Maji, kufuatia mabadiliko makubwa ya Baraza la
Mawaziri yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
jakaya Kikwete.
Kwa
mujibu wa Bw. Kimolo, miongoni mwa sababu za kujiuzulu kwake ni pamoja
na kitendo cha yeye kukashifiwa na baadhi ya wafanyibiashara wanunuzi
wa kahawa wilayani hapo, ambao walifikia hatua ya kumtamkia kuwa
hawawezi kuongea na yeye mbwa bali wanaongea na mfuga mbwa,
wakimaanisha Waziri maghembe ambaye inadaiwa alikuwa akiwakumbatia.
Kimolo,
ambaye anakuwa kiongozi wa kwanza wa wilaya kuachia ngazi katika
kipindi cha miaka 20, ya utawala wa CCM, amesema kuwa amekuwa akikosa
ushirikiano na Wizara ya Kilimo kwa ujumla juu ya msimamo wake wa
kupinga ununuzi wa kahawa mbivu (Red Cherry), kama ambavyo imekuwa
ikifanywa na baadhi ya wafanyibiashara wanaopata ridhaa toka Wizarani
humo.
Januari
7 mwaka huu, Waziri maghembe, alikutana na baadhi ya wakulima na wadau
wa zao la kahawa ambapo msimamo wa serikali ulieleza kuwa hawako tayari
kuendelea kuwaona wakulima wakiuza kahawa mbichi kwa wachuuzi hao hali
ambayo Bw. Kimolo amesema ilisababisha yeye kuonekana kutothaminiwa
msimamo wake na Serikali ya Wilaya na ya Mkoa.
Kadhalika
katika maelezo yake ya kujiuzulu, amesema kuwa kwa mujibu wa utaratibu
wa uteuzi unaofanywa na Rais, yeye uteuzi wake ulianza mwaka 2006, na
kukoma mwaka 2010 ambapo hadi sasa hakuna uteuzi mpya uliofanywa na
Rais jambo ambalo linamfanya ashindwe kupanga mikakati ya kazi kwa
maendeleo ya wilaya yake.
Amesema
kuwa, hivi sasa ni mwaka mmoja na nusu amekuwa akifanya kazi kwa
matukio ya dharura na maagizo toka juu na hivyo kumfanya aonekane
kutowajibika vilivyo katika nafasi yake na kwamba ameamua kujiuzulu
akiamini kuwa uamuzi wake utalinda heshima yake.
Aidha,
inaelezwa kuwa Bw. Kimolo amekuwa ni mtu wa karibu sana na Waziri Mkuu
Mstaafu, Edward Lowassa na kwamba kitendo chake cha kujiuzulu kina
baraka kutoka kwa kiongozi huyo mstaafu ambapo katika ziara yake
aliyoifanya hivi karibuni wilayani Momba katika mji mdogo wa Tunduma,
aliteta naye jambo muhimu.
Hata
hivyo, tetesi za kutokuwemo katika uteuzi ujao zinaelezwa kuwa ni moja
ya sababu zinazomfanya mkuu huyi kuachia ngazi mapema ili kujijengea
mazingira ya maandalizi ya kuikubali hali hiyo kabla haijatokea wakati
wa uteuzi ambao unatarajiwa kufanywa na rais wakati wowote kuanzia sasa.
Bw.
Kimolo mwenyewe, amefafanua zaidi kuhusu uamuzi wake huo akisema kuwa
kumekuwa na baadhi ya viongozi wababaishaji na kusababisha serikali
ionekane inashindwa kuwatumikia vyema wananchi na kwamba yeye ameamua
kuachia ngazi na anakwenda kushughulika na mambo yake binafsi.
Alipotakiwa
kueleza kama dhamira yake imejikita zaidi katika siasa, amesema kuwa
wakati ukifika kuingia katika mchakato wa kisiasa atafanya hivyo
kwakuwa yeye kama mtu yeyote ana uamuzi wake na katiba inamruhusu
kufanya hivyo.
"Nimechoshwa
na kejeli na mizengwe dhidi ya serikali. Wafanyibiashara wanadiriki
kusema kuwa hawako tayari kuzungumza na mbwa bali wanazungumza na
mwenye mbwa. Siwezi kufanya kazi katika mazingira ya aina hii. Wananchi
waelewe hivyo. Nitabakia kuwa raia mwema na mwananchi wa kawaida kama
wengine" alisema Bw. Kimolo.
Amesema kuwa, tayari amemuandikia barua Rais, Waziri Mkuu na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kuwajulisha juu ya uamuzi wake huo.
KWA HISANI YA HAKI NGOWI
No comments:
Post a Comment