Sunday, June 3, 2012

Jakaya Kikwete: Muungano hauvunjwi kwa kuchoma Makanisa.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete
RAIS Jakaya Kikwete amesema vitendo vilivyofanywa na wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar (JUMUKI) visiwani humo havikubaliki wala havivumiliki na kusisitiza kwamba, kuwepo au kutokuwepo kwa muungano hakuwezi kudaiwa kwa kuchoma moto makanisa.
Katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi aliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, Rais Kikwete alisema; “Haipendezi Serikali ikichukua hatua kali dhidi ya raia wake, lakini kama itashindikana haitasita kufanya hivyo. “Nawasihi viongozi na wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho kurejea kwenye madhumuni ya msingi ya jumuiya yao, wajiepushe na ajenda za kisiasa na kupandikiza chuki zitakazosababisha mifarakano baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano na baina ya Wakristo na Waislamu.” – Alisema Rais Jakaya huku akiunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ya kulaani vurugu visiwani humo.
Alisema kuwa ghasia hizo zimechochewa na viongozi wa Jumuiya hiyo ambayo ilianzishwa kwa madhumuni ya kidini, lakini hivi sasa imeacha madhumuni hayo na kubeba ajenda za siasa. Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja siku moja baada ya Kiongozi Mkuu wa Jumuiya hiyo ambaye pia anadaiwa kuwa mfadhili wa kundi hilo, Sheikh Azzan Khalid Hamdan kukamatwa na polisi visiwani humo muda mfupi baada ya kuwasili akitokea Oman.
Wakati Sheikh huyo akiwa safarini Oman, Zanzibar yalifanyika maandamano makubwa yaliyoambatana na kuchomwa moto kwa makanisa pamoja na vitu mbalimbali kuharibiwa. Katika hotuba yake Rais Kikwete alisema; “Siku za nyuma walikuwa wakitumia muda mwingi kuilaumu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa lawama hizo sasa hazisikiki.
“Tulipoanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mihadhara yao imeelekezwa kupinga Muungano na kuwakashifu viongozi waasisi wa Muungano na hata waliopo sasa.” Alisema watu hao wamekuwa wakipandikiza chuki kwa ndugu zao kutoka Tanzania bara pamoja na wafuasi wa dini ya Kikristo.
Alisema vitendo vya kuchoma moto makanisa na uhalifu haviwezi kufanywa kwa hoja ya kupinga muungano na kwamba Ukristo haukuingizwa Zanzibar na muungano bali ulikuwepo karne kadhaa kabla ya muungano na wala haukutokea Tanzania Bara.
“Kama alivyoeleza Rais Shein, ukweli ni kwamba, dini ya Kikristo kama ilivyo ya Kiislamu imeenezwa Bara kutokea Zanzibar. Kanisa kuu la Anglikana Zanzibar lilijengwa kuanzia mwaka 1873 na lile la Katoliki kuanzia 1893 ni miongoni mwa Makanisa makongwe kuliko mengi kama siyo yote kwa upande wa Zanzibar na Bara” alisema Rais Kikwete.
Alisema kuwa matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mtu kuwa huru wa kuchagua au kubadilisha dini, kwamba yanayofanywa na jumuiya hiyo kwa kisingizio cha Muungano ni jambo lisiloeleweka kabisa na wala halina mantiki na kusisitiza; “Labda kama wana ajenda nyingine”.
Aliongeza: “Jambo la kushangaza ni kutokea vurugu na ghasia wakati ambapo Serikali imetoa fursa kwa watu kutoa maoni yao kwenye mjadala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Tume ya kukusanya maoni imeshaundwa na inajiandaa kwa kazi hiyo, utaratibu mzuri umeshawekwa sasa vurugu za nini,” alihoji rais Kikwete.
Alisema kuwa hakuna sababu ya msingi kwa watu kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuwa hali hiyo inaharibu sifa na sura ya Wazanzibari na Watanzania. Alisema kuwa Watanzania ni ndugu na wamekuwa wakiishi pamoja kwa furaha licha ya tofauti zao za rangi, makabila, dini na maeneo watokako.

1 comment:

  1. Suala hili linatakiwa kuangaliwa kwa uzito wa kipekee.Kuwabebesha UAMSHO au JUMIKI suala hili ni sawa na kumbebesha Mch.Mtikila na suala lake la Mabaghacholi ambako tuliona vijana wakiingia mitaa kutaka kuvamia maduka ya waashia.Sidhani kama kuna mahala viongozi hao waliwaamrisha wafuasi hao wakachome makanisa na mabaa na wanye pombe zilizokuwa huko.Hapa tusipokuwa makini tunatengeneza kizazi kipya cha vijana ambao watakuwa na chuki ya viongozi wao wa kidini kudhalilishwa,tusisahau chuki walizokuwa nao Wazanzibar wenye asili ya Uarabu kwa jinsi wazee wao walivyoteketezwa na wanawake wao walivyolazimishwa ndoa na wengine kubakwa baada ya mapinduzi.Nadhani ni wakati muafaka wa kuwa na Tume huru ya Maridhiano Zanzibar kuliko kunyoosheana vidole.Watu wasameheane waanze upya

    ReplyDelete